Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Ikiwa Serikali ya Iran Itaanguka, Je, Putin Ataipoteza Asia ya Kati?

(Imetafsiriwa)

Habari:

Mnamo Aprili 27, shirika la habari la Vedomosti liliripoti: “Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Arakchi alitoa shukrani zake kwa Urusi na Rais Vladimir Putin kwa kuunga mkono jamhuri wakati wa mkutano mmoja jijini St Petersburg.

Putin alikutana na Arakchi jijini St Petersburg mnamo Aprili 27. Upande wa Urusi uliwakilishwa katika mkutano huo na Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov, Msaidizi wa Rais Yuri Ushakov na Mkuu wa Idara Kuu ya Ujasusi ya Jeshi Igor Kostyukov. Walioandamana na Arakchi katika mkutano huo walikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharib-Abadi na Balozi wa Moscow Kazem Dzhalali.

Putin alisisitiza kwamba Urusi itaunga mkono Iran na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba amani inaregeshwa katika eneo hilo haraka iwezekanavyo. Rais huyo pia alitaja kwamba alikuwa amepokea ujumbe kutoka kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, na akamtakia kila la kheri”.

Maoni:

Baada ya Abbas Arakchi kukataa kukutana na maafisa wa Marekani nchini Pakistan, Trump, ili kuepuka aibu zaidi alitangaza kwa kiburi chake cha kitabia, kwamba alikuwa akifutilia mbali safari ya maafisa wake kwenda Pakistan, akisema kwamba ikiwa Iran inataka kuzungumza, wangeweza “kutupigia simu” tu.

Tangu kuanza kwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani na umbile la Kiyahudi dhidi ya Iran, mamlaka za nchi hiyo zimeonyesha azma yao na kukataa kwao kukubali matakwa ya Marekani. Iran inaendelea kufuata sera huru ya kigeni kulingana na maslahi yake. Uhusiano wake na Urusi na China unatumika kama mfano wa hili.

Mara tu baada ya kuondoka Pakistan, Arakchi alizuru Urusi, na baadaye akasafiri hadi China. Urusi na China zote zinaelewa kitakachotokea ikiwa Marekani ingeleta mabadiliko ya serikali nchini Iran na kuweka serikali chini ya udhibiti wake. Ndiyo maana nchi zote mbili zinafanya kila ziwezalo kusaidia kuhifadhi utawala wa sasa nchini Iran.

Tofauti na China, Urusi inajikuta katika hali ngumu. Kwa upande mmoja, kuna makubaliano ya kimya kimya ya Putin na Trump kuhusu hatima ya Ukraine. Tangu Trump aingie madarakani, tumeona mara kwa mara jinsi Putin alivyokubaliana na maslahi ya Marekani katika masuala mengi, kwa matumaini ya kutatua vita kwa niaba ya Urusi. Lakini hadi leo, suala la Ukraine bado halijatatuliwa, na Putin anasubiri ushindi ulioahidiwa. Na ikiwa Putin sasa ataunga mkono Iran dhidi ya maslahi ya Marekani, basi hatawahi kuona ushindi nchini Ukraine ambao Trump alimwahidi.

Kwa upande mwingine, Putin anaweza kupoteza Asia ya Kati. Mashariki ya Kati imejaa kambi za kijeshi za Marekani. Isipokuwa Iran, Pakistan, Afghanistan na nchi za Asia ya Kati. Katika mradi wa Marekani wa ‘Mashariki ya Kati Kubwa’, dori maalum imepewa Pakistan, Afghanistan na nchi zote za Asia ya Kati.

Kuanguka kwa utawala wa Iran kutatumika kama njia ya Marekani kuanzisha uvamizi wa kijeshi katika eneo hilo. Kwanza, Marekani itaanzisha kambi za kijeshi katika eneo la Iran, kisha itaanza kusonga mbele zaidi katika eneo hilo, ikieneza machafuko na vurugu hadi itakapofika katika nchi za Asia ya Kati. Wakati huo, Putin hatimaye atapoteza udhibiti wa nchi za Asia ya Kati, huku Marekani ikiendelea na upanuzi wake wa kikoloni na baadaye kuelekeza mawazo yake kwa China.

Je, Putin anaelewa hili? Haiwezekani kuwa haelewi. Dola yoyote inayotaka kushawishi siasa za dunia na kuziunda kwa maslahi yake lazima iwe tishio la kweli kwa maslahi ya dola inayoongoza katika jukwaa la kimataifa, badala ya kuhakikisha usalama wake na kuendeleza maslahi yake kwa kutoa msaada—ambayo ndiyo hasa Urusi inafanya kuhusu Marekani. Dunia nzima inajua thamani ya ‘dhamana za Marekani’, na hakuna dhamana yoyote. Kwani dola inayoongoza inafuatilia maslahi yake pekee na haizingatii dola zilizo chini yake.

Waislamu! Hamu ya Amerika ya kubadilisha utawala nchini Iran haikusudii kuanzisha amani na utulivu katika eneo hilo, na yakini sio kutoa msaada kwa Waislamu katika kuanzisha utawala wa Kiislamu. Msaada wa Urusi kwa Iran si kwa maslahi ya Waislamu, bali kwa maslahi ya Urusi pekee. Kama dola za Ulaya zingeingilia kati katika eneo hilo, hazingekuwa na msaada wowote kwa Uislamu au Waislamu. Utawala wa Iran wenyewe unakwamilia katika fikra yake ya kitaifa na unapinga Uislamu au Waislamu katika eneo hilo.

Leo, nchi moja, inayowakilishwa na utawala wa Iran, imeonyesha kwamba inawezekana kusimama dhidi ya dola inayoongoza duniani, Marekani. Kwa kufanya hivyo, imeondoa dhana potofu kwamba haiwezekani kuipinga Marekani. Hata idadi kubwa ya vibaraka wa Marekani katika eneo hilo hawakufanya chochote kumsaidia Trump kuishinda Iran. Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaonyesha Waislamu leo ​​zaidi ya hapo awali kwamba yote ni juu yetu, na tunahitaji kuchukua hatua sisi wenyewe ili kusimamisha dola ya pili ya Khilafah Rashida. Na tunamuomba Mwenyezi Mungu (swt) atusaidie!

Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema katika Kitabu Chake Kitukufu:

[إِنَّ اللَّهَ لاَ يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّى يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ]  “Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao.” [13:11].

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Eldar Khamzin
Mwanachama wa Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.