Logo
Chapisha ukurasa huu

بسم الله الرحمن الرحيم

Uislamu ni Rehma na Njia ya Uokozi kwa Binadamu Kutokana na Moto wa Ubepari na Maovu Yake

(Imetafsiriwa)

Mwenyezi Mungu (swt) amemtumiliza bwana wetu Muhammad (saw) kwa ujumbe wa Uislamu kama rehma kwa walimwengu:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِلْعَالَمِينَ  “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” [Al-Anbiya: 107].

Ujumbe huu ni kuwatoa watu kutoka gizani hadi kwenye nuru, kuleta mabadiliko katika maisha ya wanadamu na kuwapa suluhisho na tiba ya matatizo yanayowakabili, na kuyafanikisha, kupitia hukmu za Uislamu na sheria zake, haki na usalama na maisha yenye staha. Rabi‘i ibn ‘Amir, Mwenyezi Mungu awe radhi naye, alifupisha hilo katika hotuba yake kwa Rustum kwa maneno mafupi yaliyojaa kina aliposema: “Mwenyezi Mungu ametutuma kuwatoa waja kutoka kwenye ibada ya waja hadi kwenye ibada ya Mola wa waja, na kutoka kwenye dhulma ya dini hadi kwenye uadilifu wa Uislamu, na kutoka kwenye ufinyo wa dunia hii hadi kwenye upana wa dunia hii na Akhera. Kwa hivyo, yeyote anayekubali hilo kutoka kwetu, tunalikubali kutoka kwake, na ikiwa hatakubali, tunakubali kutoka kwake jizyah, na ikiwa atakataa, tunampiga vita hadi tupate ushindi.”

Tukiangalia hali ya jamii ambayo Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alitumwa kwao, tunaona kwamba ilikuwa jamii ya ujinga; Watu wake walimshirikisha Mwenyezi Mungu na wakaabudu masanamu na vinyago ambavyo walivichonga kwa mikono yao kutoka kwa mbao na mawe, badala yake hata kutoka kwa tende, na waliwazika mabinti wakiwa hai, walipunja vipimo na mizani, waliamiliana na riba, na zinaa na uasherati vilienea miongoni mwao, na wenye nguvu miongoni mwao waliwadhulumu wanyonge, na ukabila na ukoo na vilio vya kimadhehebu vilienea miongoni mwao. Walimwaga damu yao kwa mikono yao wenyewe, na walipigana kati yao si kwa ajili ya jambo lolote la maana bali kwa ajili ya ukabila wenye chuki, ambapo walipigana, kwa mfano, miaka arubaini juu ya ngamia jike, na “wastaarabu” miongoni mwao walipigana katika matukio mengi kwa ajili ya maslahi yaliyohusu dola kubwa za wakati huo. Walakhmidi nchini Iraq walikuwa chini ya Wafursi, na Waghassanidi huko Ash-sham walikuwa chini ya Warumi. Kwa hivyo, iwapo Warumi wangekasirishwa na Wafursi au Wafursi na Warumi, Waghassanidi na Walakhmidi wangepigana. Kwa hivyo, waligawanyika; hakuna kilichowaunganisha, na hakuna kilichowazuia kutokana na mambo mengi mabaya.

Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kupitia Aqida ya Uislamu na hukmu zake, aliweza kuleta mabadiliko ya ubora katika maisha yao katika miaka michache katika ngazi ya mtu binafsi na katika ngazi ya pamoja. Ja‘far ibn Abi Talib anasema katika jibu lake kwa swali la Najash, “Dini hii ni ipi?”: “Tulikuwa watu wa ujinga; tuliabudu masanamu, na tulikula nyamafu, na tulifanya uasherati, na tukakata kizazi, na tulikuwa wabaya kwa majirani; wenye nguvu miongoni mwetu wangewala wanyonge. Tulikuwa juu ya hilo hadi Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na Utukufu, alipotutumia Nabii na Mtume kutoka miongoni mwetu; tunajua nasaba yake na ukweli wake na uaminifu wake na usafi wake. Kwa hivyo, alitulingania kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Nguvu na Utukufu, ili tumpwekeshe na kumwabudu Yeye, na kuacha vile ambavyo sisi na baba zetu tulikuwa tukiviabudu badala yake katika mawe na masanamu. Na alituamuru kuwa wakweli katika kauli, na kutimiza amana, na kuunganisha kizazi, na ujirani mwema, na kujiepusha na makatazo na umwagaji damu. Na alitukataza uasherati, na kusema urongo, na kula mali ya mayatima, na kuwatukana wanawake wasafi. Na alituamuru tumwabudu Mwenyezi Mungu na tusimshirikishe na chochote. Na alituamuru kwa swala na zaka na kufunga na kuhiji kwa yeyote mwenye uwezo wa kufika huko. Kwa hivyo, tulimwamini, na tulikuwa na imani naye, na tukamfuata kwa yale aliyoleta. Kwa hivyo, tulimwabudu Mwenyezi Mungu pekee na hatukumshirikisha na chochote, na tukaharamisha aliyotuharamishia sisi, na tukahalalisha aliyotuhalalishia sisi.” Uislamu uliwahamisha Waarabu kutoka kuwa wachungaji wa kondoo hadi viongozi wa mataifa, na ukawafanya kuwa watu wa sababu na wabebaji wa ujumbe wa kheri na haki kwa ulimwengu, wakivumilia madhara na mateso kwa ajili yake.

Athari ya ulinganizi wa Uislamu haikuishia kwa Waarabu au kwa Bara Arabu pekee. Ulinganizi wa Uislamu ni ulinganizi wa ulimwengu wote, na Mwenyezi Mungu (swt) alimtuma Mtume Wake (saw) na wito huu kwa watu wote. Mola wetu, Mwenye Nguvu na Utukufu, anasema: [وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيراً وَنَذِيراً ] “Na hatukukutuma ila kwa watu wote, uwe mbashiri, na mwonyaji.” [Saba: 28].

Uislamu ulienea na watu wakaingia humo kwa wingi kutoka matabaka, makabila na rangi tofauti tofauti. Kisha, kwa kuasimashwa kwake kwa Dola ya Kiislamu mjini Madina, hukmu za Uislamu zilitekelezwa kivitendo katika uhalisia wa maisha, na Waislamu na wasiokuwa Waislamu kutoka kwa raia wa dola waliishi chini yake maisha ya heshima, na dunia ikang'aa kwa nuru ya Mola wake, na falme mbili zenye nguvu zaidi wakati huo, Fursi na Rumi, zilishindwa. Waislamu waliendelea katika ushindi na kueneza Uislamu hadi walipobadilisha sura ya historia, na jambo hilo likabaki hivyo hadi kufutwa kwa Dola ya Khilafah.

Kisha baada ya Dola ya Khilafah kufutwa na hukmu za Uislamu kutotekelezwa tena katika uhalisia wa maisha, ukandamizaji ulirudi kuifunika dunia nzima, na wanadamu wote, si Waislamu pekee, walirudi kuishi maisha ya shida na taabu chini ya mfumo wa kibepari na hadhara yake haribifu, ambayo hutenganisha dini na maisha na imejengwa juu ya ukoloni na kunyonya damu ya watu na kuiba utajiri wao na kuwaacha wakiteseka na umaskini, njaa na magonjwa; kanuni inayofanya faida na mali kuwa na thamani kubwa zaidi kuliko kitu chochote, na kila kitu chini yake kimekuwa chini ya uuzaji na ununuzi, hata mwanadamu ambaye Mwenyezi Mungu alimheshimu na kumtungia sheria zinazomhifadhia maisha yake na utajiri wake na heshima yake, na kuhakikisha utekelezaji wake kupitia dola ambayo inaweza kuhamasisha jeshi ikiwa Muislamu atashambuliwa. Siasa katika Uislamu ni utunzaji wa mambo, na Dola ya Uislamu ni dola ya utunzaji na si dola ya utozaji ushuru kama ilivyo kwa dola za kibepari na wafuasi wao kutoka kwa watawala katika nchi zetu, ambao huchukua viti kama njia ya ufujaji na uporaji na kuiba riziki ya watu, bila kusahau kwamba hawabaki juu yake isipokuwa kama wanatekeleza maslahi na miradi ya mabwana zao wa kikoloni, wa kwanza miongoni mwao ni Amerika. Katika upande wa kijamii, kumetokea ufisadi na kuzorota kwa maadili ambapo hadhara ya Magharibi umemwachilia mtu binafsi ili kukidhi silika zake apendavyo, hivyo mahusiano yaliyokatazwa yameenea, na ushoga umehalalishwa, na ukiukwaji wa asili ya ndani umekuwa uhuru ambao lazima uheshimiwe. Labda kile kilichovuja kutoka kwa hati na taarifa na ushuhuda kuhusu kisiwa cha Epstein kinafupisha ufisadi wa hadhara ya Magharibi na mateso ya wanadamu chini yake. Dunia inatawaliwa na uchafu uliovunda, na hadhara ya Magharibi na uhuru wake vimeleta uharibifu kwa watu wake kabla ya watu wengine.

Wanadamu leo ​wanahitaji mtu wa kuwaokoa kutoka kwa hadhara ya kibepari, wanahitaji mtu wa kuwaokoa kutoka kwa ukoloni na sheria ya msitu, wanahitaji mtu wa kuwapa usalama na maisha yenye heshima. Hakuna mwingine isipokuwa Uislamu na hukmu zake unaoweza kufanya hivyo, na hakuna mwingine isipokuwa Dola ya Khilafah ambayo itatekeleza hukmu hizi kivitendo katika uhalisia wa maisha unaoweza kuwapeleka wanadamu kwenye ufuo wa usalama.

Kwa hivyo, wajibu wa Waislamu ni kutekeleza dori yao katika kubeba ujumbe wa Uislamu na kufanya kazi kwa dhati ili kusimamisha Khilafah Rashida ya pili kwa njia ya Utume, ambayo itauokoa ulimwengu kutokana na maovu ya ubepari na ugumu na taabu chini yake. Hakuna fursa kubwa kuliko mwezi wa Ramadhan ya kunoa azma, kujadidisha agano na Mwenyezi Mungu, na kufanya kazi ya kutekeleza Sheria Yake, na kukifanya Kitabu Chake kilichoteremshwa katika mwezi huu mtukufu kuwa mahali pa utekelezaji, katiba na mfumo kamili wa maisha kwa Waislamu na uhai kwa watu wote.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Bara’ah Manasrah

Template Design © Joomla Templates | GavickPro. All rights reserved.